Serikali imesema utekelezaji wa Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu (LTPP) 2025 umeleta maboresho makubwa katika ubora wa maisha ya Watanzania, hali inayoonekana kupitia kuongezeka kwa wastani wa umri wa kuishi na kuboreshwa kwa huduma za afya.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo Jumatatu, Februari 2, 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema wastani wa umri wa kuishi kwa Mtanzania umeongezeka kutoka miaka 51 mwaka 2000 hadi kufikia miaka 68.3 mwaka 2022.
Ameeleza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuboreshwa kwa huduma za afya, ikiwemo kupungua kwa vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 750 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2000 hadi vifo 104 mwaka 2022.
Profesa Mkumbo amesema kwa ujumla maboresho hayo yanaonesha kuimarika kwa ustawi wa jamii, mifumo ya utawala na utoaji wa huduma za msingi kwa wananchi, hatua inayothibitisha matokeo chanya ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya muda mrefu nchini.
Chanzo; Mwananchi