Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzani, Wolfgang Pisa, ametangaza marufuku kwa watumishi wa kanisa hilo kushiriki katika kampeni za siasa.
Akiongea katika misa ya kuadhimisha miaka mia moja ya seminari ya Kipalapala-Tabora, leo amesema:-
"Mtawa, Padri au kiongozi yeyote wa kanisa hapaswi kushiriki katika kampeni zozote za siasa. Wala hapaswi kutambulishwa na chama chochote kwa kuvalishwa gwanda lolote la chama chochote cha siasa au kiashiria chochote."
"Ni Marufuku Mapdri, marufuku kwa watawa, marufuku kwenu nyinyi waseminaristi kuonekana kwenye kampeni ya siasa, marufuku kubwa," amesema Askofu Pisa.
Tamko hili linakuja ikiwa ni siku moja baada ya picha iliyosambaa ikiwaonesha Masista wa kituo cha Masista wa Mtakatifu Benedicto wa Msaada wa Kikristo Afrika kutoka Ndanda, wakionekana katika mkutano wa kampeni wa Chama Cha Mapinduzi, huko Masasi, Mtwara wakiwa wameshikilia machapisho mbalimbali ya kampeni za CCM.
Katika hotuba yake Pisa ameonya juu ya kuvaa mavazi kama kofia au Tsheti za vyama vya siasa.
Chanzo: Nipashe