Wananchi wa Jiji la Mwanza wamejitokeza mbele ya Tume Huru ya Uchunguzi wa machafuko yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 mwaka jana, kwa lengo la kutoa ushahidi na maelezo kuhusu matukio hayo.
Machafuko hayo yanadaiwa kusababisha vifo vya watu kadhaa, kujeruhiwa kwa wengine pamoja na uharibifu wa mali mbalimbali.
Akizungumza leo jijini Mwanza, mjumbe wa tume hiyo ambaye pia ni kiongozi wa timu ya uchunguzi, Balozi Ombeni Sefue, amesema kuwa tume imefika mkoani humo kwa lengo la kuzungumza na wananchi waliopatwa na madhira katika tukio hilo. Ameeleza kuwa wananchi wanapaswa kuwa huru kutoa taarifa zao bila woga wowote, kwani tume imejipanga kusikiliza kwa uwazi na haki.
Sefue ameongeza kuwa lengo kuu la tume ni kubaini chanzo cha adha na madhira yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29 mwaka jana, ili kupata ukweli wa kilichosababisha machafuko hayo.
Aidha, amesema kuwa tume hiyo imegawanyika katika makundi matatu kwa ajili ya kutembelea maeneo mbalimbali yaliyokumbwa na machafuko. Kwa sasa wapo Jijini Mwanza, na baadaye watatembelea mikoa ya Geita na Mara kuendelea na zoezi hilo la uchunguzi.
Chanzo; Clouds Media