KiongoziI Mkuu wa Kanisa la Ngurumo ya Upako Jijini Arusha, Nabii Mkuu GeorDavie Moses, ameteuliwa kuwa Mwakilishi na Balozi wa Amani wa Afrika Mashariki kupitia Shirika la Mabalozi wa Amani la Umoja wa Mataifa (UN-PAF) lenye makao yake makuu Jijini New York, Marekani.
Taarifa kutoka Marekani zinaeleza kuwa uteuzi huo ulifanywa rasmi na Mwenyekiti wa Dunia wa UN-PAF, Balozi Kingsley Ossai, ambaye ametuma barua maalumu za utambulisho kwa Serikali ya Tanzania, United Nations Chapter ya Tanzania pamoja na Ubalozi wa Marekani nchini, kwa lengo la kumtambulisha Nabii GeorDavie katika wadhifa wake mpya.
“Tunatambua mchango wa Nabii GeorDavie katika kueneza amani na maendeleo ya kijamii. Tunaamini kama Balozi wa Amani Duniani, ataziwakilisha vema nchi za Afrika Mashariki kupitia Shirika letu,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.
Nabii Mkuu GeorDavie, ambaye pia ni mlezi wa JMAT Taifa, amekuwa akihusishwa kwa muda mrefu na shughuli za kijamii, ikiwemo kusaidia vijana na familia kujikwamua kiuchumi na kielimu. Kupitia huduma zake za kiroho na kijamii, amejipatia sifa kubwa ndani na nje ya Tanzania.
Uteuzi huo unamfanya kuwa miongoni mwa viongozi wachache wa kidini kutoka Afrika Mashariki waliopata nafasi ya kutambulika kimataifa kupitia taasisi inayohusiana na Umoja wa Mataifa katika masuala ya amani, upendo na maendeleo endelevu.
“Nitaitumikia Afrika Mashariki kwa moyo wa upendo, mshikamano na amani. Ni heshima kubwa kwa Tanzania,” amesema Nabii GeorDavie baada ya uteuzi huo.
Chanzo; Clouds Media