Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameishauri Serikali kurejesha utaratibu wa kutoa vibali vya watu wanaotakiwa kutumia vilevi ili kudhibiti matumizi holela kama inavyoonekana kwa sasa kisiwani humo.
Hayo yameelezwa leo Jumanne, Februari 17, 2025 wakati wa kipindi cha maswali na majibu katika mkutano wa 11 wa Baraza la Wawakilishi unaoendelea Chukwani, Unguja Zanzibar.
Mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohamed Ali Suleiman amesema Serikali haioni umuhimu wa kuweka utaratibu wa kutoa vibali maalumu kwa wanaotaka kunywa, ili kuepusha athari zinazoweza kutokea ikiwamo vilevi kutumika holela na hata kwa vijana wadogo.
Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Idrissa Mustafa Kitwana amesema kwa kuwa baraza ndilo lenye jukumu la kutunga sheria basi wakiona linafaa wanaweza kulipeleka ili kuhakikisha jambo hilo linatekelezwa.
Katika swali la msingi, Dk Mohamed amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la uingizaji wa kilevi kinachojulikana kama Double Kick kwa siku za karibuni Zanzibar, kinyume na sheria ya vileo namba 9 ya mwaka 2020.
Amesema kilevi hicho kina zaidi ya asilimia 43 ya alcohol, jambo linalosababisha athari kubwa kwa vijana wanaokitumia akitaka kujua kiwango kipi Serikali inalitambua tatizo hili la uingizwaji wa kilevi hicho.
Chanzo; Mwananchi