Mtoto mwenye umri wa miaka saba, mwanafunzi wa darasa la pili, anadaiwa kubakwa na mwanaume mmoja anayefahamika kwa jina la Frank maarufu kama Bangazoo, ambaye ni konda wa magari katika stendi ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa maelezo ya mlezi wa mtoto huyo, tukio hilo linadaiwa kutokea wakati mtoto alipokwenda kuchukua nyasi katika moja ya mashamba yaliyokuwa yakivunwa. Inadaiwa kuwa mtuhumiwa, ambaye ni jirani yao, alimuita mtoto huyo na kisha kumuingilia kimwili kabla ya kutoroka eneo la tukio.
Viongozi wa kijiji hicho wametoa wito kwa Jeshi la Polisi kuchukua hatua za haraka dhidi ya watuhumiwa wa matukio ya ukatili wa kijinsia mara tu taarifa zinapopokelewa.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Afisa Maendeleo na Ustawi wa Jamii, Agnes Kesi, amewahimiza wananchi kuendelea kuripoti matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa wahusika.
Chanzo; Crown Media