Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kimempa Mchungaji Godfrey Malisa anayekabiliwa na kesi mbili ikiwamo ya uhaini, uwakilishi wa jopo la mawakili watano.
Mbali na kesi ya uhaini, Malisa anakabiliwa na kesi nyingine ya makosa ya kimtandao iliyoanza kusikilizwa jana Februari 12,2026 na Hakimu Mkuu Mkazi, Ally Mkama wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Februari 13,2026, Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwabukusi, ametaja jopo la mawakili hao kutoka Chapter ya Kilimanjaro ni Leonard Mashabara, Deogratias Matata, Elisante Kimaro, Moonlight Tupa na Fredy Kimaro.
"Kwa pamoja jana wameingia katika shauri la jinai Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi linalomkabili ndugu Godfrey Malisa," amesema.
"Shauri hilo lipo mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Mkama, liliendelea katika hatua ya usikilizwaji na shahidi mmoja wa upande wa mashtaka aliweza kutoa ushahidi wake na hatimaye kesi imeahirishwa hadi Februari 20,2026 ambapo itaendelea na usikilizwaji," ameongeza Wakili Mwabukusi
Juzi Februari 11,2026 shauri hilo lilikwama kusikilizwa baada ya Malisa kuomba Mahakama iahirishe akisubiri msaada wa kisheria kutoka TLS, ombi ambalo lilikubaliwa na Mahakama kwa masharti kuwa juhudi za kuhakikisha mshtakiwa anapata uwakilishi zifanyike ili kesi ianze kusikilizwa.
Chanzo; Mwananchi