Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba amepiga marufuku matumizi ya dhamana katika utoaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri, baada ya kubaini kuwa mfumo wa kibenki unaotumika kwenye baadhi ya maeneo kwa majaribio umeanza kukwamisha walengwa kutokana na masharti ya hati za nyumba na wadhamini wa serikali ambayo wafanyabiashara wadogo hawana uwezo nayo.
Dkt. Mwigulu ametoa maelekezo hayo Bungeni jijini Dodoma wakati wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu, akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Segerea, Agnesta Lambat, aliyetaka Serikali ibadilishe mfumo wa ukopeshaji wa fedha za asilimia 10 kupitia mabenki kwa kuwa una masharti magumu kwa wafanyabiashara ndogondogo.
“Mchinga hawezi kuwa na hati ya nyumba, ukimwambia alete hati ya nyumba ndiyo apewe mkopo ni dhahiri hata hatakuwa nayo. Na maeneo mengine walitakiwa watoe barua ya udhamini wa watumishi waliopo serikalini, na yenyewe mchinga, bodaboda waanze kutafuta mtumishi aliyepo serikalini amdhamini ni tatizo jingine. Maelekezo niliyoyatoa waondoe hayo masharti yanayokwamisha walengwa hao,” amesema Dkt. Mwigulu Nchemba – Waziri Mkuu wa JMT.
Chanzo; Millard Ayo