Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linamshikilia Shabani Buruhani Kidunda (37), Askari Mgambo na mkazi wa Chogo, Wilaya ya Handeni, kwa tuhuma za kumjeruhi kwa risasi Abdallah Ally (35), dereva wa bajaji na mkazi wa eneo hilo.
Kwa Mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga ACP Almachius Muchunguzi, tukio hilo limetokea tarehe 02 Februari 2026 majira ya saa 2:30 usiku katika Sheli ya Mount Meru, Chogo Stendi, Kata ya Mdoe, Tarafa ya Chanika, Wilaya ya Handeni. Inadaiwa mtuhumiwa alifyatua risasi kwa kutumia bunduki aina ya rifle na kumjeruhi majeruhi katika maeneo la tumboni na kiganja cha mkono wa kulia.
Uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa tukio hilo lilitokana na uzembe na utani kati ya wahusika.
Mjeruhi amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni kwa matibabu zaidi, huku hali yake ikielezwa kuwa inaendelea vizuri.
Mtuhumiwa bado anashikiliwa na Jeshi la Polisi na atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limetoa wito kwa wananchi wanaomiliki silaha kuhakikisha wanazingatia sheria na kanuni za umiliki na matumizi sahihi ya silaha ili kuepuka madhara yasiyo ya lazima.
Chanzo; Clouds Media