Jumla ya vitabu vya Amali 18,354 vimesambazwa katika shule zote za serikali na binafsi zinazofundisha mkondo wa Amali nchini ambako kwa kidato cha kwanza vimetolewa 15,780 na kidato cha pili ni 2,574.
Akikabidhi vitabu hivyo leo Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dk. Aneth Komba amesema, serikali imetoa vitabu hivyo kwa shule zote za umma na binafsi ili kuongeza hamasa katika ufundishaji na ujifunzaji wa masomo hayo yatakayosaidia kukabiliana na changamoto ya ajira kwa mwanafunzi pindi wanapohitimu.
Amesema, mwaka 2024 serikali ilianza kutekeleza mtaala ulioboreshwa ambao umegawanyika katika mkondo wa Amali na wa jumla, akisisitiza kwamba mkondo wa Amali lengo lake ni kujenga elimu ujuzi kwa mwanafunzi.
"TET imetoa mafunzo kwa wakuu wa shule wote kuhusu maboresho yaliyofanyika kwenye mtaala hasa katika mkondo wa Amali, pamoja na namna ya kutumia maktaba mtandao ambako vitabu vyote hupatikana," amesema.
Pia ameongeza kwa kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizowezesha upatikanaji wa vitabu nchini, hasa vitabu vya Amali ambavyo vinagawiwa bure kwa shule zote nchini za serikali na binafsi.
Mkuu wa shule ya ufundi Nzega na Makamu Mwenyekiti wa wakuu wa shuke Tanzania Bara Mwl. Mwanakombo Martin amesema vitabu hivyo vitasaidia katika ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi na kuleta tija katika utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa katika mkondo wa Amali.
Chanzo; Nipashe