Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limefanikiwa kumkamata mtu mmoja aitwaye Denis Ogesa (28) mkazi wa Nairobi nchini Kenya, kwa tuhuma za kuvunja na kuingia katika tawi la benki ya Azania iliyopo katika mji wa Namanga wilayani Longido.
Akitoa taarifa hiyo leo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amesema mtuhumiwa huyo alitenda tukio hilo Januari 14, 2026 muda wa saa 6:40 usiku.
SACP Masejo amebainisha kuwa wakati mtuhumiwa huyo akiendelea kutekeleza tukio hilo la kihalifu katika benki hiyo, alikamatwa akiwa tayari na fedha za Tanzania zenye thamani ya Tshs 91,280,000/= na fedha za Kenya zenye thamani ya Kshs 288,700.
Jeshi la Polisi mkoani humo limesema linakamilisha uchunguzi kuhusiana watu alioshirikiana nao ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Chanzo; Bongo 5