Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametoa siku saba kwa watu wote waliojipatia ardhi kwa njia zisizofaa kurejesha maeneo hayo kwa wamiliki halali kabla ya kuanza kuwataja hadharani.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa mkoa wa kupunguza migogoro ya ardhi ambayo imeshamiri kwa kiasi kikubwa katika Jiji la Dar es Salaam.
Pia, Chalamila ametoa onyo kali kwa watu waliopatiwa dhamana ya kusimamia mirathi ya watoto wa marehemu, akionya kuwa yeyote atakayejaribu kujimilikisha mali hizo kinyume cha sheria hatabaki salama.
Amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia vitendo vya dhuluma dhidi ya watoto waliofiwa na wazazi wao na kwamba sheria itachukua mkondo wake kwa wale wote watakaobainika kukiuka maadili ya usimamizi wa mirathi.
Katika jitihada za kuleta suluhu ya kudumu, Mkuu wa Mkoa amefungua milango ya ofisi yake kwa muda wa wiki moja kuanzia sasa kwa wananchi wote wenye matatizo ya ardhi.
Amewataka kufika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakiwa na nyaraka zote muhimu ili kusaidia mchakato wa utatuzi wa migogoro hiyo kisheria na kwa uwazi.
Chanzo; Itv