Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya limetoa ufafanuzi kufuatia taarifa zinazosambazwa mitandaoni kuhusu kifo cha Peter Mwita Wanda, mkazi wa Sabasaba Tarime, aliyekuwa akishikiliwa kwa tuhuma za unyang’anyi wa kutumia silaha.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa Disemba 31, 2025, na baada ya kufikishwa kituoni alianza kulalamika kujisikia vibaya, hali iliyopelekea askari kumkimbiza katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime kwa ajili ya matibabu ya dharura.
Mtuhumiwa huyo alifariki dunia Januari 1, 2026, akiwa anaendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo, ambapo uchunguzi wa kitabibu ulibaini kuwa chanzo cha kifo chake kilikuwa ni tatizo la upungufu wa damu.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi limetoa onyo kali kwa watu wenye tabia ya kuandaa na kusambaza taarifa za upoteshaji kwenye mitandao ya kijamii, likisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za nchi na hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Chanzo; Mwananchi