Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja lilifanya Operesheni kuanzia tarehe 31 Januari 2026 ambapo katika Operesheni hiyo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 13 wanaohusika kwa wizi wa vifaa vya ujenzi kwa njia ya udanganyifu, Wahalifu wa Unyang'anyi kwa kutumia silaha na matapeli wa fedha.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 03 Februari 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Richard Thadei Mchomvu wakati akizungumza na vyombo vya habari huko ofisini kwake Madema.
Amesema baadhi ya wezi hutumia namba za simu kuwapigia wauzaji wa vifaa vya ujenzi kama wateja na wanapofika eneo la ujenzi(site) huwatapeli wauzaji hao.
Kamanda mchomvu amewataja watuhumiwa wanaohusika na wizi wa vifaa vya ujenzi kuwa ni
(1) Ali Maulid Ali, miaka 29, MshirazI wa Mwanyanya (2) Salum Omary Abed, miaka 37, Mmakonde wa Mwanyanya (3) Abdallah Kombo Khamis, miaka 28, MshirazI wa Mwakaje, (4) Mudathir Said Khamis, miaka 22, MshirazI wa Mwanyanya, (5) Hamadi Iddi Mishim, miaka 35, MshirazI wa Bububu (6) Suleiman Idd Mishim, miaka 35, MshirazI wa Kama, Wote Wilaya ya Magharibi A"
Hata hivyo ametoa wito kwa wamiliki wa maduka kuchukua tahadhari dhidi ya wezi hao na kuhakikisha wanalipwa kwanza kabla ya kufikisha mzigo kwenye eneo husika.
Katika hatua nyingine Kamanda Mchomvu amesema Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa wengine sita (06) wanaounda kikundi cha kihalifu maarufu kama "Battery Low" ambao wanajihusisha na matukio mbalimbali ya kihalifu ikiwemo unyang'anyi kwa kutumia silaha na mashambulio ya kudhuru mwili.
Watuhumiwa hao walifanya matukio yenye kuleta hofu kwa jamii na kujificha katika msitu wa Welezo uliopo Wilaya ya Magharibi A" Mkoa wa Mjini Magharibi. Upelelezi wa watuhumiwa hao unaendelea, hata hivyo juhudi za kumkamata kiongozi anaefadhili kikundi hicho zinaendelea.
Chanzo; Crown Media