Kikosi cha nane cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (TANBAT 08), kinacholinda amani Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kimetunukiwa nishani za ulinzi wa amani na Umoja wa Mataifa (UN) kutokana na mchango wake mkubwa katika operesheni ya kulinda amani Nchini humo chini ya mwamvuli wa MINUSCA.
Katika sherehe ya gwaride la heshima iliyofanyika tarehe 06 Septemba 2025 mjini Berberati, Wanajeshi zaidi ya 500 wa TANBAT 08 wametunukiwa nishani hizo ikiwa ni ishara ya kutambua michango yao katika kuwalinda Raia, kusaidia shughuli za kibinadamu na kuimarisha utulivu katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro.
Uvishwaji wa nishani hizo uliongozwa na Naibu Mkuu wa Vikosi vya Kulinda Amani vya Umoja wa Mataifa nchini CAR, Meja Jenerali Maychel Asmi ambaye ndiye alikuwa Mgeni rasmi katika hafla hiyo ambapo katika hotuba yake Meja Jenerali Asmi ametoa pongezi kwa Uongozi, nidhamu na mshikamano mkubwa uliodhihirishwa na TANBAT 08 wakati wa operesheni zao.
Chanzo: Millard Ayo