Ikwa imepita miezi mitatu tangu aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humprey Polepole, anayedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana, familia yake imefika katika nyumba aliyokuwa amepanga eneo la Ununio, jijini Dar es Salaam, ili kukusanya mali za ndugu yao.
Leo, Jumanne, Januari 6, 2026, familia hiyo, mbali na kukusanya vitu vya ndugu yao, pia wamesoma sala maalumu ya kumuombea Polepole, aliyewahi kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kabla ya kuzungumza na vyombo vya habari.
Polepole alidaiwa kutekwa usiku wa Jumatatu, Oktoba 6, 2025, akiwa nyumbani kwake eneo la Ununio. Kadhia hiyo ilitokea miezi michache tangu kutangaza kujiuzulu nafasi ya ubalozi wa Tanzania nchini Cuba, Julai 13, 2025.
Jumanne, Agosti 5, 2025, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kupitia Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Balozi Samwel Shelukindo, ilieleza kuwa imepokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka, ikitaarifu Rais Samia Suluhu Hassan juu ya mambo aliyoyajua, na ametengua uteuzi wa Polepole kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba na kumwondolea hadhi ya ubalozi.
Chanzo; Mwananchi