Kesi ya Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu itaendelea kusikilizwa mfululizo kuanzia Jumatatu hadi Oktoba 24 mwaka huu.
Hayo yameamuliwa na Mahakama Kuu nchini humo wakati Lissu alipokuwa akisikiliza mashtaka yanayomkabili ya uhaini. Hayo yanajiri ikiwa ni wiki chache kabla ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki kufanya uchaguzi mkuu ambao chama cha Lissu CHADEMA hakitoshiriki.
Tundu Lissu ambaye alishika nafasi ya pili katika uchaguzi uliopita wa urais mwaka 2020, alikamatwa mwezi Aprili na kushtakiwa kwa uhaini kufuatia kauli yake ambayo waendesha mashtaka walisema ilikuwa ya uchochezi ikiwataka wananchi kuasi na kuvuruga uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29.
Tundu Lissu na chama chake cha CHADEMA waliapa kutoshiriki uchaguzi huo hadi kutakapofanyika mageuzi muhimu katika mchakato mzima wa uchaguzi wakisema kuwa mfumo wa sasa unakipendelea Chama Cha Mapinduzi (CCM) cha Rais Samia Suluhu Hassan, ambacho kimekuwa madarakani tangu 1961 Tanzania,ikijulikana kama Tanganyika wakati huo ilipopata uhuru.
Chanzo: Dw