Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknoloya imetoa ahueni kwa wanafunzi waliofeli katika mitihani yao ya kidato cha pili na sasa badala ya kukariri darasa, watafanyiwa programu maalumu huku wakiendelea na kidato cha tatu.
Ahueni hiyo imetangazwa leo Jumamosi Januari 10, 2026 na Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa katika taarifa yake aliyoitoa kwa umma.
Hatua hiyo inakuja ikiwa ni saa chache zimepita tangu Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya kidato cha pili ambapo jumla ya wanafunzi wa shule 705,091, sawa na asilimia 86.93, wamefaulu kuendelea na kidato cha tatu kwa kupata daraja la kwanza hadi la nne ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.52 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2024.
Kamishna wa Elimu amesema: “Ninaelekeza kwamba wanafunzi ambao hawakufikia alama za ufaulu za kidato cha pili, mwaka 2025 waendelee na kidato cha tatu mwaka 2026 badala ya kukariri (kurudia) kidato cha pili.
“Wanafunzi hao watapewa programu maalumu rekebishi (remedial programme) itakayotolewa wakati wakiendelea na masomo yao ya kidato cha tatu,” amesema Dk Mtahabwa.
Chanzo; Mwananchi