Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Camillus Wambura amewataka watanzania wote kushiriki katika jukumu la udhibiti na usimamizi wa Silaha ili kulinda Nchi ikiwa ni utekelezaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
IGP Wambura ameyasema hayo leo Februari 3, 2026 Jijini Dar es Salaam wakati akizindua Kamati ya Udhibiti na Usimamizi wa Silaha pamoja na kufungua Kikao cha kwanza cha Kamati hiyo kinachofanyika kwa siku tatu ambapo zitawasilishwa mada mbalimbali za kuwajengea uwezo wana kamati ili kufahamu majukumu yao, sheria na kanuni, itifaki za kikanda na kimataifa zitakazo waongoza katika jukumu la kudhibiti na kusimamia silaha na risasi nchini.
Amesema, Changamoto ya uzagaaji wa silaha haramu kwa kiasi kikubwa ulitokana na migogoro kwa baadhi ya nchi zinazoizunguka Tanzania, kuwepo kwa mipaka isiyo rasmi na ukiukwaji wa sheria.
Aidha, alisema changamoto hiyo ilikuwa kubwa katika miaka ya 2000 kurudi nyuma kutokana na machafuko yaliyokuwa yanaendelea nchi jirani lakini kutokana na kuboreshwa kwa mikakati ya udhibiti na usimamizi wa silaha,tatizo hilo limepungua kutokana na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na vyombo vya usalama.
Chanzo; Crown Media