Wakulima na wafugaji katika wilaya ya Songea mkoani Ruvuma wametakiwa kufuata sheria na taratibu za matumizi ya ardhi ili kuepusha migogoro, ikiwemo kuacha tabia ya kuchukua sheria mikononi mwao pindi mifugo inapovamia mashamba ya kilimo ambapo tarehee 27/9/2025 mwenyekiti wa kijiji cha Chiurungi kilichopo halmashauri ya wilaya ya Songea amejeruhiwa vibaya na wafugaji na kulazwa katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) katika hospitali ya Mt Joseph Peramiho baada ya kupigwa na wafugaji waliopeleka mifugo yao katika mashamba.
Akiongea na wananchi wa kijiji cha Chiurungi mara baada ya kutokea tukio la mwenyekiti kushambuliwa na wafugaji mkuu wa wilaya ya Songea Mhe Wilman Kapenjama Ndile amesema kuwa tayari Jeshi la Polisi limewakamata watuhumiwa wanaohusishwa na tukio hilo, na ameagiza hatua kali zichukuliwe dhidi yao ili kutoa fundisho kwa wengine na kuzuia matukio kama hayo yasijirudie.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa kijiji cha Chiurungi wamelalamikia tabia ya baadhi ya wafugaji kupeleka mifugo yao mashambani kwa makusudi, hali inayosababisha uharibifu mkubwa wa mazao na migogoro ya mara kwa mara wamesema kuwa wanapojaribu kuwakemea wafugaji hao, hukumbana na vipigo na vitisho.
Afisa mifugo wa halmashauri ya wilaya ya Songea, Erick Kahisi, amesema kijiji cha Chiurungi hakijatenga eneo la malisho ya mifugo, na serikali inafahamu kuwa kijiji hicho hakina wafugaji wakazi ameeleza kuwa mifugo inayosababisha migogoro hiyo inatoka katika vijiji vya jirani.
Chanzo: Clouds Media