Wakati wananchi na wakazi wa nyumba za Kikwajuni Mjerumani, Mkoa wa Mjini Magharibi wakiwa bado na malalamiko kuhusu mikataba ya kuondolewa katika eneo hilo, Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), limesema litaanza kuzibomoa nyumba hizo Machi 26, 2026, kupisha utekelezaji wa mradi wa mji wa kisasa.
Wananchi hao wamesema mikataba waliyopewa na Shirika la Nyumba haina vigezo vya kutosha, licha ya baadhi yao kuitwa kwenda kusaini, wakibainisha kuwa baadaye waligundua inaweza kuwageuka kutokana na kukosa vipengele muhimu vya kisheria.
Eneo hilo lina jumla ya nyumba 150 zilizojengwa na Wajerumani wakati wa kipindi cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume na kugawiwa wananchi bila malipo. Kati ya nyumba hizo, 99 zinamilikiwa na ZHC huku 51 zikiwa ni mali binafsi.
Hata hivyo, katika mipango ya serikali ya kuendeleza miji na kujenga nyumba za kisasa kutokana na uchakavu wa nyumba hizo kupitia Shirika la Nyumba Zanzibar, eneo hilo linatarajiwa kukabidhiwa kwa mwekezaji anayetarajiwa kujenga nyumba zaidi ya 1,150.
Katika makubaliano yaliyopo kati ya ZHC na wananchi wanaoishi katika nyumba hizo, imeelezwa kuwa wananchi watapatiwa fedha za kujikimu kwa kipindi cha miaka miwili wakati mradi ukiendelea, kisha watapatiwa nyumba za kuishi katika eneo hilo baada ya mradi kukamilika. Hata hivyo, ujenzi wa mradi huo umetajwa kutekelezwa ndani ya mwaka mmoja.
Chanzo; Mwananchi