Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amewaonya wananchi wanaofunga fedha kama shada la maua kwa ajili ya zawadi kwa wapendwa wao katika msimu wa Sikukuu ya Wapendanao (Valentine), akisema kitendo hicho ni ukiukwaji wa sheria na kinachangia uharibifu wa noti za taifa.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Crown Media jana, Alhamisi, Februari 12, 2026, ofisini kwake jijini Dodoma, Tutuba amesema fedha ni tunu ya taifa inayopaswa kutunzwa, huku akibainisha kuwa kuzibandika kwa gundi na kuzikunja wakati wa kutengeneza mashada husababisha kuchakaa na kuchanika mapema.
Amesema uharibifu huo hulazimisha BoT kuchapisha fedha mpya mara kwa mara ili kuziba pengo, hatua inayoongeza gharama kwa taifa.
“Hizi fedha tunazichapisha kwa gharama kubwa. Zinapobandikwa gundi na kukunjwa hovyo, zinachakaa mapema; hivyo BoT inalazimika kuchapisha fedha mara kwa mara. Kama unataka kumpa zawadi ya Valentine mpendwa wako, mnunulie bidhaa yenye thamani au mpatie fedha hizo zikiwa katika hali yake ya kawaida,” amesema Tutuba.
Aidha, amesisitiza kuwa kila anayeshika fedha ya Tanzania ana wajibu wa kuzitunza na kuzihifadhi, kwa kuwa ni miongoni mwa alama na tunu muhimu za taifa.
Onyo hilo linakuja wakati kukiwa na ongezeko la mitindo ya zawadi za Valentine, ikiwamo mashada ya fedha, pipi, na bidhaa nyingine…
Chanzo; Mwananchi