Familia ya kijana Michael Rambau (18), mkazi wa Mtaa wa Karikacha, Kata ya Rau, mkoani Kilimanjaro, imekumbwa na butwaa baada ya kupata taarifa ya kijana wao aliyekamatwa na Jeshi la polisi mkoani humo kuwa amejiua kwa kujinyonga ndani ya chumba cha mahabusu.
Kijana huyo ambaye ni fundi bomba na dereva bodaboda maarufu katika mtaa huo, anadaiwa kukamatwa na Jeshi la Polisi Januari 13, 2026 kwa madai ya kuhusika na tukio la kumjeruhi baba mdogo wake wakati wakigombania spana kwenye gari la marehemu baba yake, aliyefariki Novemba 22, 2025.
Taarifa za kujiua kwa kijana huyo, zimetolewa na Kamanda wa Polisi mkoani humo, Simon Maigwa ambaye amesema kijana huyo alijiua kwa kujinyonga akiwa ndani ya mahabusu ya polisi Moshi kati Januari 13, 2026.
Akizungumza baba mdogo wa kijana huyo ambaye ni msemaji wa familia hiyo, Today Rambau, amesema wameshangaa kupata taarifa za kijana wao kujiua kwa kujinyonga kituo cha polisi hali ambayo amesema imewapa mshituko.
Aidha, amesema kuhusu tukio la kijana huyo (marehemu) kumshambulia baba mdogo wake, amesema Januari 12 kijana huyo (marehemu) alitofautina na baba yake mdogo wakati alipochukua spana za gari kwenye gari la marehemu baba yake ambaye alifariki Novemba 22, mwaka jana.
Chanzo; Mwananchi