Zaidi ya safari za ndege 1,400 kwenda, kutoka, au ndani ya Marekani zilifutwa Jumamosi baada ya mashirika ya ndege kuagizwa kupunguza safari za anga kufuatia kufungwa kwa serikali ya nchi hiyo.
Hatua hiyo imeathiri maelfu ya wasafiri na kusababisha usumbufu mkubwa katika viwanja vikuu vya ndege nchini humo.
Kwa mujibu wa tovuti ya ufuatiliaji wa safari za ndege, FlightAware, karibu safari 6,000 pia ziliahirishwa Jumamosi, baada ya zaidi ya safari 7,000 kuahirishwa siku ya Ijumaa.
Hali hiyo imesababisha misururu mirefu ya abiria na kuchelewesha ratiba za safari katika maeneo mengi ya Marekani.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga (FAA) ilitangaza mapema wiki hii kwamba itapunguza shughuli za safari za anga kwa hadi asilimia 10 katika viwanja 40 vya ndege vyenye shughuli nyingi zaidi nchini humo.
Uamuzi huo umechukuliwa kutokana na uchovu unaowakabili wadhibiti wa safari za anga, ambao wamekuwa wakifanya kazi bila malipo tangu kufungwa kwa serikali kuanza tarehe 1 Oktoba.
Taarifa kutoka FAA zinaeleza kuwa idadi ndogo ya watumishi waliopo kazini imeathiri uwezo wa mamlaka hiyo kusimamia kwa ufanisi trafiki ya anga, jambo lililolazimu mashirika ya ndege kupunguza idadi ya safari ili kuhakikisha usalama wa abiria.
Wakati huo huo, Warepublican na Wademocrat bado hawajakubaliana kuhusu njia ya kumaliza mkwamo uliosababisha kufungwa kwa serikali.
Mazungumzo katika Bunge yameendelea bila mafanikio makubwa, huku kila upande ukilaumu mwingine kwa kuchelewesha suluhisho.
Kufungwa kwa serikali kwa muda mrefu kunaendelea kuathiri sekta mbalimbali nchini Marekani, zikiwemo usafiri wa anga, huduma za umma, na uchumi kwa jumla.
Mashirika ya ndege yameonya kuwa, iwapo hali hiyo itaendelea, huenda usafiri wa anga ukakumbwa na usumbufu mkubwa zaidi katika siku zijazo.
Chanzo; Global Publishers