Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera linaendelea na uchunguzi wa tukio la mauaji ya mwanamke mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30, Sophia Zakalia, mfanyabiashara wa ndizi na mkazi wa Kata ya Katoma, Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, mwili wa marehemu ulikutwa umetupwa shambani, hali iliyozua taharuki miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, SACP Blasius Chatanda, amesema mwili wa marehemu ulipatikana jana ukiwa umefungwa kwa kamba, huku sehemu zake za siri zikionesha dalili za kuingiziwa kitu butu, jambo linaloashiria ukatili mkubwa.
Kamanda Chatanda ameongeza kuwa uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mauaji hayo huenda yalifanywa kwa nia ya kulipiza kisasi, na kwamba jeshi la polisi linaendelea kuwatafuta watu wanaohusishwa na tukio hilo.
Amesisitiza kuwa Polisi ina uhakika wa kuwabaini na kuwakamata wahusika ndani ya muda mfupi ili sheria ichukue mkondo wake.
Chanzo; Global Publishers