Wakulima wa kijiji cha Kimana mkoani Manyara wamelalamikia uvamizi wa mashamba yao na wafugaji wanaodai maeneo hayo ni ya malisho, hali inayosababisha migogoro ya mara kwa mara.
Wakulima hao wanasema wamekuwa wakizuiwa kulima, kufukuzwa mashambani na hata mazao yao kuliwa na mifugo, licha ya maeneo hayo kutambuliwa kisheria kuwa ni ya kilimo na makazi kwa mujibu wa mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Wakizungumza na Waandishi wa habari, wakulima hao wamedai kuwa Mkuu wa Wilaya aliwahi kuahidi kukutana nao ili kutafuta suluhu ya mgogoro huo, lakini hakufika ofisini siku iliyopangwa, jambo lililowalazimu baadhi yao kumfuata.
Wakulima hao wamesema wameishi na kulima katika maeneo hayo kwa zaidi ya miaka kumi, wamejenga makazi, kulea familia na kusomesha watoto, lakini sasa wanaishi kwa hofu na kukosa haki mbele ya wafugaji wanaotumia nguvu bila kufuata sheria.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya amesema kuwa alipata dharura iliyomzuia kufika kukutana na wakulima kama ilivyopangwa, lakini amesema amepokea malalamiko yao na tayari anayafanyia kazi na ameahidi kukutana na wakulima hao siku ya kesho Jumamosi akiwa na timu ya wataalamu ili kusikiliza pande zote na kutafuta suluhu ya kudumu itakayolinda haki za wakulima na kuondoa migogoro kati ya wakulima na wafugaji katika eneo hilo.
Chanzo; Millard Ayo