Ukiitazama siasa ya dunia kwa sasa, hasa kwa taswira ya nchi za Magharibi utagundua kuna kitu kimoja kinachofanana. Sera za ya kujitenga na kuzuia raia wa mataifa yanayoonekana kama ni tegemezi kuingia kwenye nchi hizo imepamba moto, nchi za Ulaya zimeenda mbali zaidi kwa kutengeneza vikosi vya kuzuia wahamiaji wanaoitwa haramu ambao asilimia kubwa wanatoka kwenye mataifa ambayo yana machafuko yaliyosababishwa na nchi hizo hizo za magharibi.
Hata hivyo ukigeuka upande wa mashariki hasa nchi ya Urusi utaona kitu tofauti kabisa. Sera inayoonekana kutumika zaidi ni ya kuiunganisha dunia. Utaligundua hii kwa kuangalia idadi ya makongamano na mikutano ya kujenga uhusiano inayofanyika ndani na nje ya Urusi ikihusisha mataifa mbalimbali duniani kwa lengo la kutengeneza umoja.
Huenda mwezi Septemba umeweka rekodi ya kusanyiko linaloweza kuibadili kwa ukubwa taswira ya dunia kwa miaka inayokuja. Hii ni baada ya jiji la Niznhy Novrogod kuwakaribisha vijana 2000 toka mataifa mbalimbali dunia kwenye kongamano maalum la vijana lililopewa jina la World Youth Forum Assemby 2025. Vijana kutoka nchi 120 zenye mila, desturi na tamaduni tofauti waliweza kukutana kwa pamoja kupata mafunzo na kubadilishana ujuzi ili kuweza kutengeza dunia mpya ya vijana wenye malengo yanayofanana.
Wazungumzaji mbalimbali waliweza kutoa mafunzo na kuendesha mijadala iliyogusa mada tofauti kwa washiriki kama ubunifu na sanaa, utawala wa umma, ujasiriamali, michezo, elimu na sayansi, dijitali na teknolojia ya habari. Haikuishia tu kuwasikiliza washiriki waliweza pia kuuliza maswali na kutoa maoni yanayoakisi mitazamo yao.
Upatikanaji wa ajira imekuwa ni changamoto kubwa kwa vijana wa mataifa hasa ya nchi za Afrika, ilitia moyo kuona namna kampuni ya Avito ilivyoweza kutoa mafunzo ya namna kijana anaweza kujiandaa kuingia kwenye soko la ajira na vitu vya kuzingatia ili kuonyesha utofauti wake. Kwa washiriki wa kongamano hili waliotokea Afrika na baadhi ya mataifa ya Asia hii ilikuwa ni moja ya mada zilizowavutia sana na pengine ni kitu ambacho klabu za WYF kwa Afrika zinapaswa kukitilia mkazo.
Kupitia kongamano hili kwa pamoja vijana walikubaliana kuanzishwa kwa kituo cha kimataifa cha maudhui (international content centre) kitakachotoa mafunzo ya mara kwa mara na kutoa taarifa ikiwa ni pamoja na kuzungumzia fursa kwa vijana zinazopatikana nchini Urusi. Kwa jicho la kawaida hii inaweza kuonekana ni kitu cha kawaida, lakini ukiiangalia kidiplomasia hii ni hatua kubwa kwenye kutengeneza ushirikiano uliojengwa kwenye misingi ya kuwatafutia fursa vijana. Kwa ushirikiano wa manguli wa habari toka Urusi na Global Fact Checking Network (GFCN) vijana waliweza kufundishwa namna ya kutengeneza maudhui yenye mvuto, kutumia mtandao wa umakini na kujifunza namna ya kuzitambua taarifa potoshi.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi inayosimamia Kongamano hili (WYF Directorate) ndugu Dmitry Ivanov akizungumzia hatua hii alisema kituo hiki kitatumika kubadilishana ujuzi kwa wadau wa vyombo vya habari lakini pia kuhamasisha maudhui chanya miongoni mwa vijana wa mataifa tofauti ili kulinda mila na tamaduni za kila taifa.
Mjadala mwingine uliovutia ulikuwa ni ule ulioandaliwa na African Initiative News Agency ukiwa na kaulimbiu ya “Mapinduzi ya Simulizi: Namna ya Kukwepa Makelele ya Taarifa” (Story Revolution: How to Cut Through the Information Noise) mjadala uliojikita katika kubadilishana ujuzi wa namna gani kila jamii inaweza kutumia mbinu za simulizi katika kusambaza taarifa chanya zinazoihusu na kufanya zifike mbali katika zama hizi ambazo kuna mlundikano wa taarifa mtandaoni, hasa upande wa TikTok ambako kuna vijana wengi zaidi.
Pengine mjadala mkubwa ulikuwa ni ule uliohusisha matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence) kwenye utengenezaji maudhui. Ilivutia namna mijadala yote ambayo ilihusisha mada hii iliweza kuvuta hisia za washiriki kwa kuzingatia kuwa wanufaika na wahanga wa Akili Unde ni kundi la vijana. Katika moja ya mjadala, Mikhail Zvinchuk ambaye ni Mkuu wa Russian Rybar Think Tank alisema ni wakati wa sasa mataifa mengine duniani kuangalia mfano wa Urusi na kutengeneza mpangokazi wa maudhui yanayokabiliana na upotoshaji wa mataifa au watu wenye nia mbaya. Aliongeza kuwa kwa sasa ni rahisi kwa watu kudanganyika kwani mitandao inatumia mfumo wa algorithm na kuwalisha kile wanachotaka kukisikia hivyo kuwapunguzia tabia ya kuhoji vitu visivyoendana na imani zao.
Kwa siku 5 nilizokuwepo Niznhy Novgorod naweza kuwa shuhuda wa kusema Urusi imeamua kuwa sehemu sahihi ya historia kwa kuliunganisha kundi ambalo linaijenga kesho ya dunia, nikimaanisha kundi la vijana. Kwa kutoa maagizo ya kuendelezwa kwa World Youth Festival mara baada ya kufanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2024, Rais wa Urusi Vladimir Putin atakumbukwa kwa hatua hii, kwani kama mipango na matarajio yakitimia, tutashuhudia ushirikiano zaidi wa vijana nchi tofauti wanaokubaliana katika kuona dunia inakuwa na msingi wa umoja badala ya kuendekeza mifarakano na kujitenga kama tunavyoshuhudia kwa sasa.
Hakika hiii ilikuwa ni Septemba ya kukumbukwa.