Jeshi la Polisi mkoani Morogoro, linamsaka Helakumi Kacheri kwa tuhuma za kumuua mkewe, Sofina Elipisini (27), mkazi wa Singisa, wakiwa shambani, huku chanzo kikidaiwa kuwa wivu wa kimapenzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, amesema mtuhumiwa alimuua mkewe kwa kumshambulia na silaha yenye makali sehemu mbalimbali za mwili, akimtuhumu kuendeleza uhusiano na mzazi mwenzake wa awali.
Amesema baada ya mtuhumiwa kutekeleza mauaji hayo, alikimbia, na Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Diwani wa Singisa, Anna Mgela, amesema tukio hilo limetokea Januari 4, 2026 katika kitongoji cha Tindegela, kata ya Singisa, wilayani Morogoro, na kwamba alipata taarifa kutoka kwa mtendaji wa kijiji walichokuwa wakiishi.
“Nikiwa kwenye kikao, nilipigiwa simu na mtendaji wa kijiji na kunipa taarifa za mauaji haya, sikuweza kufika eneo la tukio, badala yake nilimuagiza mtendaji atoe taarifa polisi. Baada ya polisi kufika, waliuchukua mwili. Hata hivyo, mtuhumiwa hakupatikana kwa sababu baada ya kufanya hivyo alikimbia,” amesema Mgela.
Chanzo; Mwananchi