Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amesema lugha ya Kiswahili inaendelea kuimarika kimataifa na kuwa mhimili wa utambulisho wa Afrika pamoja na chombo muhimu cha kukuza diplomasia, elimu na maendeleo.
Makonda ameyasema hayo Februari 20, 2026 alipohutubia Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Lugha-Mama yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Umoja wa Mataufa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) jijini Paris, Ufaransa, ambapo aliwakilisha Serikali ya Tanzania.
Amesema zaidi ya watu milioni 500 duniani wanazungumza Kiswahili, jambo linalothibitisha nafasi ya lugha hiyo kama nyenzo ya kimkakati katika diplomasia na uchumi wa kimataifa.
“Kuenea kwa Kiswahili duniani kunafungua fursa mpya za ushirikiano wa kimataifa, biashara na kubadilishana maarifa, huku kikibaki kuwa nguzo ya utambulisho wa Waafrika,” amesema Makonda.
Katika hotuba yake, Makonda pia aliwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa UNESCO kwa mchango wake katika kukuza Kiswahili duniani.
Chanzo; Mwananchi