Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na taasisi ya Aspire Educational Technologies wa United Arab Emirates wamesaini hati ya Makubaliano ya Ushirikiano wa miaka mitatu kati ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa ajili ya kukuza elimu nchini katika eneo la maudhui ya kidigitali.
Makubaliano haya ya utiaji saini yamefanyika katika makao makuu ya ofisi za TET Jijini Dar es salaam. Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba akizungumza katika hafla hiyo amesema kuwa tukio hilo linaashiria mwanzo wa ushirikiano wa kimkakati na kuwa makubaliano hayo yamekuja kwa wakati muafaka ambapo serikali imeanza kutekeleza mtaala ulioboreshwa, ambao unasisitiza matumizi ya TEHAMA na teknolojia nyinginezo katika ufundishaji na ujifunzaji kuanzia darasa la awali.
“Hii kwetu imekuja wakati mzuri kwani kwa sasa mtaala ulioboreshwa unasisitiza kukuza stadi za Karne ya 21 kwa wahitimu zikiwemo ubunifu, kutatua matatizo, uzalendo, fikra tunduizi, ushirikiano na ujuzi wa kidigitali. Makubaliano haya yamelenga kujenga stadi hizi hususani stadi ya ujuzi wa kidigitali” amesema Dkt. Komba.
Makubaliano hayo yatahusisha ushirikiano wa pamoja kati ya Aspire na TET kwa ajili ya kuandaa maudhui ya elimu ya kidigitali kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini Tanzania ikiwemo Taasisi ya Aspire Educational kuandaa maudhui ya kidigitali yenye ubora wa hali ya juu, yanayoendana na mtaala kwa ajili ya wanafunzi wa shule za sekondari, kwa mujibu wa miongozo na viwango vya TET.
Aidha, kwa upande wa TET ni kuwezesha mchakato wa kuidhinisha maudhui yote yaliyotayarishwa na Aspire ili kuhakikisha yanaendana na mtaala pamoja na viwango vya elimu nchini. Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Aspire Rahul D’ Mello ameeleza kuwa wamefurahi kupata nafasi ya kufanya ushirikiano huo ambao anaamini utaweza kuleta tija katika elimu nchini Tanzania.