Zaidi ya wagonjwa 500 mkoani Songwe wamefanikiwa kurejeshewa uwezo wao wa kuona baada ya kupatiwa matibabu ya mtoto wa jicho kupitia kambi maalum ya siku sita.
Kambi hiyo imeandaliwa na Shirika la Kimataifa la Helen Keller kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka hospitali za rufaa za Mbeya na Songwe, ambapo huduma hiyo imetolewa bure kwa wananchi waliojitokeza kwa wingi.
Mwakilishi wa TAMISEMI, Dkt. Kalidushi Kubingwa, amepongeza ushirikiano huo kati ya serikali na wadau, akisisitiza kuwa mpango huo ni mkombozi kwa Watanzania wenye changamoto za kuona.
Baada ya mafanikio hayo mkoani Songwe, huduma hiyo inatarajiwa kuhamia mkoani Tabora, huku wanufaika wakitoa shukrani kwa kurejeshewa matumaini ya kuona tena na kuendelea na shughuli zao za kila siku.
Chanzo; Mwananchi