Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala limethibitisha kutokea kwa ajali ndogo ya ujenzi katika jengo lililopo Mtaa wa Aggrey, Kariakoo, ambapo watu kadhaa wamejeruhiwa baada ya mbao na milunda kuanguka kutoka kwenye jengo lenye zaidi ya ghorofa 10.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Oktoba 7, 2025, Kamishna Msaidizi wa Jeshi hilo, Peter Mabusi, amesema tukio hilo lilitokea leo saa 11 jioni na kuhusisha jengo lililokuwa likijengwa katika eneo hilo.
“Ni kweli tukio limetokea Kariakoo lakini sio jengo kuanguka kama ilivyodaiwa awali. Ni mbao na milunda tu iliyokuwa kwenye ujenzi ambayo ilianguka na kujeruhi baadhi ya watu waliokuwa chini,” amesema Mabusi.
Ameongeza kuwa mtu mmoja alinaswa chini ya milunda hiyo lakini alifanikiwa kuokolewa akiwa hai, na hakuna vifo vilivyoripotiwa.
Kwa sasa, Jeshi la Zimamoto linaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo pamoja na kuchukua hatua za kuhakikisha usalama unaimarishwa katika majengo yanayoendelea kujengwa, hasa yenye shughuli nyingi za kibiashara kama Kariakoo.
Chanzo: Mwananchi