Taharuki na sintofahamu imetanda katika Mtaa wa Igodima jijini Mbeya baada ya mkazi wa eneo hilo anayedaiwa kuwa mwalimu na mwanafunzi wa Chuo Kikuu, Zainabu Mwalyepelo, kukutwa amefariki dunia nyumbani kwake.
Taharuki hiyo imetokea leo Alhamisi Januari 15, 2026 katika eneo hilo baada ya baba mzazi wa marehemu, Jacob Mwalyepelo kufika nyumbani hapo na uongozi wa serikali ya mtaa huo kubomoa mlango na kukuta mwili kwenye sofa.
Akizungumza huku akitokwa machozi, Mwalyepelo amesema ni maumivu makali kumpoteza mtoto wake ambaye amehangaika naye kwa muda mrefu na gharama kubwa kwa matibabu.
Amesema mwanaye alikuwa mwalimu kitaaluma na alikuwa akijiendeleza kielimu katika Chuo Kikuu cha Catholic Mbeya (CUoM).
"Naumia jamani, bora ningekufa mimi niliyezeeka, nimehangaika sana na mwanangu kuanzia India, Hospitali ya Rufaa Kanda, leo mtoto wangu anakufa, nifanyeje," amesema.
Akimzungumzia mdogo wake, kaka wa marehemu, Christopher Mwalyepelo amesema mdogo wake hakuwa na mume wala mtoto na alikuwa akisumbuliwa na tatizo la moyo na wakati mwingine kubanwa na kifua.
Amesema kwa muda ambao alitoka hospitali hakupenda kukaa sehemu ya kelele, hali iliyomfanya kuwa mwenyewe nyumbani kwake katika mtaa huo.
Chanzo; Mwananchi