Ikiwa ni takribani wiki mbili tangu Jeshi la Polisi limkamate John Heche ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, Wakili wake, Hekima Mwasipu amesema kiongozi huyo anatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kigaidi, muda wowote atafikishwa mahakamani.
Wakili Mwasipu amesema tuhuma za ugaidi zilizoibuliwa kwa mteja wake zinahusiana na fujo wakati wa maandamano yaliyotokea Oktoba 29, 2025 eneo la Kimara hadi Magomeni, jijini Dar es Salaam wakati wa uchaguzi mkuu.
Leo Jumatano Novemba 5, 2025 akizungumza na Mwananchi Wakili Mwasipu amesema baada ya kuelezwa tuhuma zake alikataa kuhojiwa hadi wawepo mawakili wake.
"Anatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kigaidi, matukio yaliyotokea Kimara Dar es Salaam hadi Magomeni, Polisi wamesema wana ushahidi anahusika na muda wowote anaweza kupelekwa mahakamani," amesema.
Kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram, Chacha Heche ambaye ni mdogo wake Heche aliandika jana Jumanne kwamba Heche amefikishwa Dar es salaam.
Mwananchi mara kadhaa imemtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro kujua kinachoendelea lakini simu yake ilikuwa ikiita pasina kupokewa.
Chanzo; Mwananchi