Wakati watu wakiendelea kujiuliza wapi alipo aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) nalo limejitokeza na kulitaka Jeshi la Polisi kuchunguza na kuweka wazi kilichotokea.
Pia, jukwaa hilo limehoji tabia hizi za kutekana zimetoka wapi wakati ambao Tanzania ni nchi ya amani.
Polepole anadaiwa kutekwa Oktoba 6, 2025 na watu wasiojulikana wakati ambao jeshi la Polisi likisema linaendelea kufanyia kazi madai hayo.
Kufuatia hilo, taarifa kwa vyombo vya Habari iliyotolewa leo Jumanne Oktoba 8, 2025 na TEF imesema tukio hili linawakumbusha Watanzania matukio yaliyotangulia ya utekaji ya vijana Mdude Nyagali, Deusdedit Soka na wenzao.
“Jamii haijasahau pia mauaji ya kikatili ya Mzee Ali Kibao katika kipindi kifupi kilichopita,” imesema taarifa hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa TEF, Deudatus Balile.
Wakati ndugu wa Polepole wakisema ametekwa akiwa Ununio, Dar es Salaam, Jeshi la Polisi kupitia Msemaji wake, David Misime amesema wamepokea taarifa hizo na wanafanya uchunguzi.
Chanzo: Mwananchi