Majeruhi aliyepata ajali ya basi iliyotokea jana majira ya saa 12 asubuhi, mkoani Lindi, Ahmad Ally amefariki dunia baada ya kupata ajali katika eneo la Mavuji, wilayani Kilwa mkoani humo wakati akipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Ally anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 40-50, amefariki dunia katika ajali iliyotokea saa 7 usiku wa kuamkia leo Jumapili Februari 8, 2026 ambapo ajali ya awali ilitokea Jumamosi ya Februari 7, 2026, saa 12 asubuhi na kusababisha vifo vya watu wawili, akiwamo mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.
Akizungumza kwa njia ya simu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilwa (Kinyonga), Dk. Reornad Lucas, amesema hospitali hiyo ilipokea mwili wa marehemu saa 7 usiku pamoja na majeruhi wawili, ambao walitibiwa na baadaye kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa (Sokoine).
Daktari huyo amesema kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kilwa (Kinyonga), huku majeruhi wakihamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi (Sokoine).
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi (Sokoine), Dk. Alexander Makalla, amesema marehemu ametambuliwa kwa jina la Ahmad Ally na alikuwa akipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Hata hivyo Dk. Makalla amesema marehemu alikuwa akisafirishwa kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi, lakini walipofika eneo la Mavuji, wilayani Kilwa, dereva wa ambulance aliacha njia na kuingia porini na kusababisha ajali hiyo.
Chanzo; Millard Ayo