Search

Saved articles

You have not yet added any article to your bookmarks!

Browse articles

GDPR Compliance

We use cookies to ensure you get the best experience on our website. By continuing to use our site, you accept our use of cookies, Privacy Policy, and Terms of Service.

Mwalimu Aliyechapa Wanafunzi Video zikasambaa, Afukuzwa Kazi

Uongozi wa Shule ya Sekondari Makumbusho iliyopo Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam umemuondoa kazini mwalimu Felix Msila baada ya kuonekana akiwachapa viboko wanafunzi kikatili.

Siku chache zilizopita ilisambaa picha mjongeo katika mitandao ya kijamii ikimuonyesha mwalimu huyo wa kujitolea akiwachapa wanafunzi kwa mtindo ambao uliibua hisia tofauti kwa wananchi, huku aliekuwa akirikodi video hiyo akisikika akisema kwa uchungu kwamba kijana huyo hafai kuwa mwalimu.

Mmoja wa wanafunzi walioangushiwa kichapo kutoka kwa mwalimu huyo ni Khatibu Salimu wa kidato cha pili, huku Halmashauri ya Kinondoni ikiahidi kuchukua hatua zaidi.

Aidha, kwa mujibu wa barua ambayo imeonwa na Nipashe Digital yenye kumbukumbu namba Kumb/No/KMC/MKSS/ Vol.01, Mwalimu Msila Felix ameondolewa kazi Septemba 19, 2025 na Mkuu wa Shule ya Sekondari Makumbusho, Ester Mianga.

Barua iliyotumwa kwa mwalimu huyo imesomeka "kutokana na tukio ulilolifanya la kutoa adhabu kikatili kwa mwanafunzi wa kidato cha pili Salim Septemba 18, mwaka huu bila kuzingatia waraka wa elimu namba 24 wa mwaka 2002 kuhusu utoaji wa adhabu ya viboko shuleni, uongozi wa shule kwa kushirikiana na kamati ya wazazi umekufukuza kazi rasmi kuanzia leo Septemba 19, 2025."

Barua hiyo ilipelekwa nakala kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Ofisa Elimu Sekondari, mwenyekiti wa bodi ya shule na mwenyekiti wa kamati ya wazazi.

 

Chanzo: Nipashe

Kuhusiana na mada hii: