Wakati Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari akieleza kuwa Serikali inaangalia uwezekano wa kumchukulia hatua Mange Kimambi kwa tuhuma za kuhamasisha Watanzania kuandamana, baadhi ya wanasheria wamesema suala hilo si rahisi kisheria.
Wataalamu hao wamesema ni vigumu kwa nchi kama Marekani kumkabidhi mtu kwa nchi nyingine, hususan pale anapokabiliwa na tuhuma zenye mwelekeo wa kisiasa, hata kama kuna mikataba ya ushirikiano au makubaliano ya kiuhamisho kati ya mataifa hayo.
Johari alitoa kauli hiyo alipowasili katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali jijini Dodoma, ambako pia alifanya mazungumzo na wafanyakazi wa ofisi hiyo, jana muda mfupi baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo.
Akizungumza baada ya kuwasili ofisini kwake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johari, alisema kuwa ofisi yake inaendelea kuangalia uwezekano wa kumkamata mwanadada aliyeko nje ya nchi, akimaanisha Mange Kimambi, ikiwa ni pamoja na kutumia mikataba maalumu ya ushirikiano iliyopo kati ya Tanzania na Marekani.
Chanzo; Mwananchi