Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amewataka viongozi katika mikoa yote nchini kuhakikisha hakuna kijana anayezuiwa au kuambiwa hana sifa ya kunufaika na mikopo ya Sh. bilioni 200 iliyotengwa na Serikali kwa ajili ya kuwawezesha vijana kiuchumi.
Nanauka alitoa agizo hilo jana alipokuwa akizungumza katika Jukwaa la Vijana wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati (Vijana Platform Campus Connect) mkoani Singida, jukwaa linalowaunganisha vijana kutoka makundi mbalimbali wakiwemo wanafunzi, waendesha bodaboda na bajaji, wamachinga pamoja na vijana wengine wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi.
Alisisitiza kuwa jukumu la viongozi wa Serikali si kuwakatisha tamaa vijana, bali kuwasaidia kufikia vigezo vinavyohitajika ili waweze kupata mikopo hiyo.
“Kijana akifika ofisini asiambiwe hana sifa. Kazi ya kiongozi ni kumsaidia kama hana sifa, aelekezwe na kuandaliwa ili afikie vigezo vya kupata mkopo, siyo kumrudisha nyuma,” alisema Nanauka.
Aidha, alieleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi wakati wa kampeni kutenga Shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wa kati, wadogo na kampuni changa (startups) ili kuinua uchumi wao. Fedha hizo zimeelekezwa katika wizara za kisekta ili kuhakikisha zinawafikia vijana kulingana na maeneo wanayojishughulisha nayo.
Hatua hiyo inalenga kuongeza ushiriki wa vijana katika uchumi, kuchochea ubunifu na kupunguza changamoto ya ajira nchini.
Chanzo; Eatv