Wizara ya Afya imetoa tahadhari kwa wananchi kuhusu ongezeko la magonjwa ya mlipuko yakiwemo mafua makali ya Influenza, UVIKO-19, homa ya Dengue na Kipindupindu na kutoa wito kwa jamii kuzingatia kikamilifu hatua za kinga ili kudhibiti maambukizi.
Taarifa hiyo imetolewa leo Februari 25,2026 na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Grace Magembe amesema takwimu za ufuatiliaji zinaonesha kuwa kila mwaka kati ya mwezi Novemba hadi Aprili kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wa mafua makali na UVIKO-19 nchini na duniani.
Amesema magonjwa hayo ya huambukizwa kwa njia ya hewa na husambaa kwa njia ya matone madogo yanayotoka kwa mtu mwenye maambukizi anapokohoa, kupiga chafya au kuzungumza, na yanaweza kusababisha homa kali, kikohozi, maumivu ya kichwa na mwili, mafua pamoja na uchovu.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Magembe amewataka wananchi kufunika pua na mdomo wanapokohoa au kupiga chafya, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono, kuepuka misongamano isiyo ya lazima na kuvaa barakoa wanapokuwa na dalili au wanapokaribiana na wenye dalili.
Chanzo; Nipashe