Watu wawili wamefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa baada ya kupigwa na radi katika Kitongoji cha Mbesi, Kijiji na Kata ya Utengule, Halmashauri ya Mlimba, Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, tukio hilo limetokea usiku wa Februari 23, 2026, wakati waathirika hao walipokuwa njiani wakitoka kutembea.
Waliofariki dunia ni Tano Lunasi (36) na Ngimila Mashana (27), na kwamba wote ni wakulima na wakazi wa Mbesi.
Waliojeruhiwa ni Manyanda Masasila (35) na Michael Msanga (26), ambao walipatiwa matibabu na kuruhusiwa kurejea nyumbani.
Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuchukua tahadhari wakati wa msimu huu wa mvua ili kuepuka madhara yanayoweza kusababisha vifo.
Chanzo; Nipashe