Wanaume 127 kati ya 165 waliofanyiwa uchunguzi wa mabusha mwezi huu jijini Dar es Salaam wamegundulika kuwa na ugonjwa huo.
Hata hivyo 27 kati ya waliogundulika kuwa na mabusha tayari wamefanyiwa upasuaji na wanaendelea vizuri.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 8, 2026 wakati wa kutangaza kambi ya uchunguzi na ufanyaji upasuaji wa mabusha bure iliyoanza Januari 5, 2026, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Mohamed Mang'una amesema wagonjwa hao waligundulika baada ya kufanya uchunguzi katika kambi hiyo inayoendelea.
Amesema katika kambi hiyo, watafanya uchunguzi na upasuaji bure hadi Januari 30, 2026.
"Baada ya muda huo, wale watakaohitaji kufanyiwa upasuaji wataendelea na utaratibu wa kuchangia kama kawaida," amesema.
Akizungumza hali ya ugonjwa huo ulivyo, amesema tatizo lipo sana katika mikoa ya ukanda wa Pwani kuanzia Mtwara.
Chanzo; Mwananchi