Jeshi la Polisi nchini limethibitisha kumkamata Ambrose Dede, mlinzi wa Kampuni ya Ulinzi ya African Safari ambaye pia mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kwa tuhuma za kupanga na kuhamasisha vitendo vya uhalifu kupitia kundi la WhatsApp linaloitwa Sauti ya Watanzania.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Novemba 12, 2025 na Msemaji wa Jeshi la Polisi ,David Misime Dede amekamatwa akiwa maeneo ya njia Panda ya Makiungu, Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.
Taarifa ya Misime imeeleza kuwa, uchunguzi wa awali unaonyesha mtuhumiwa huyo ni miongoni mwa viongozi wa kundi hilo la WhatsApp (Group Admins), akishirikiana na watu waliopo ndani na nje ya nchi kupanga na kuendeleza mpango wa kufanya uhalifu kwa kivuli cha maandamano ya amani.
Kamanda Misime amesema uchunguzi unaendelea ili kuwapata watuhumiwa wengine wanaohusishwa na mtandao huo wa mawasiliano, huku namba nyingine zikihifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi.
“Baada ya kukamilika kwa uchunguzi, hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa, tunawataka wananchi kuepuka kushiriki katika makundi ya mtandaoni yanayopanga au kuhamasisha vitendo vya uvunjifu wa amani,tunasisitiza kuwa yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria bila kuonewa, imeeleza taarifa ya Misime.
Chanzo; Nipashe