Search

Saved articles

You have not yet added any article to your bookmarks!

Browse articles

GDPR Compliance

We use cookies to ensure you get the best experience on our website. By continuing to use our site, you accept our use of cookies, Privacy Policy, and Terms of Service.

Wakubaliana Kutokuoa Wanawake Waliokeketwa

Baadhi ya wanaume wa jamii ya Kimasai katika Wilaya ya Monduli mkoani Arusha wameadhimia kwa pamoja kutooa wanawake waliokeketwa kama hatua ya kupinga na kudhibiti vitendo vya ukeketaji dhidi ya watoto wa kike.

Azimio hilo limetolewa jana katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji yaliyofanyika kitaifa katika Kijiji cha Losirwa, Kata ya Esilalei, wilayani humo.

Akizungumza kwa niaba ya wanaume hao, kiongozi wa kimila (Laigwanani) Yamati Laizer amesema wamefikia uamuzi huo ili kuunga mkono juhudi za kukomesha ukeketaji, akibainisha kuwa kama wanawake wa jamii hiyo walivyokubali kuachana na mila hiyo, sasa wanaume nao wamechukua msimamo wa kutomuoa mwanamke atakayebainika kufanyiwa ukeketaji.

Makole Laizer, mmoja wa washiriki wa azimio hilo, amesema wamepatiwa elimu kuhusu madhara ya ukeketaji na wataendelea kuhamasishana ndani ya jamii ili kuondoa kabisa vitendo hivyo.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima, amesema jamii kwa ujumla—ikiwemo vijana, wanaume, viongozi wa dini, viongozi wa mila na wanahabari—wanapaswa kupaza sauti kupinga ukeketaji dhidi ya wanawake na watoto wa kike.

Ameeleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau imeimarisha utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), kupitia Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto zipatazo 18,618 katika ngazi za mikoa, halmashauri, kata, vijiji na mitaa nchi nzima.

Kwa upande wake, Msaidizi wa Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Dk. Majaliwa Marwa, amesema ukeketaji ni ukiukaji wa haki za binadamu na hauwezi kuhalalishwa kwa misingi ya kitamaduni, kijamii au kidini.

 

 

Chanzo; Nipashe

Kuhusiana na mada hii: