Nyumba zaidi ya 52 zimebomoka huku nyingine zikiezuliwa paa kufuatia mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali katika kijiji cha Makanjiro, wilayani Ruangwa mkoani Lindi.
Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea anayekaimu Wilaya ya Ruangwa, Mohamed Hassan Moyo, alisema tukio hilo limesababisha madhara makubwa kwa wakazi wa eneo hilo, huku familia nyingi zikibaki bila makazi.
Moyo amesema Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa inaendelea kufanya tathmini ili kubaini kiwango cha madhara yaliyosababishwa na mvua na upepo huo, ili serikali iweze kutoa msaada stahiki kwa waathirika.
Aidha, amewaomba wananchi wa kijiji cha Makanjiro kuwahifadhi kwa muda wananchi waliopoteza makazi yao wakati serikali ikiendelea na juhudi za haraka za kuwapatia msaada wa dharura.
Chanzo; Eatv