Mhudumu katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Simon Ruhinda amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma kwa tuhuma za mauaji ya Rhoda Mobe, mkazi wa Kijiji cha Burunga, Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Ruhinda (55) ameunganishwa na watuhumiwa wengine wawili ambao ni Mwita Maginga (47), mkazi wa Tarime na Marco Maginga (45) ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi jijini Mbeya, wote walifikishwa katika Mahakama hiyo kwa mara ya kwanza Desemba 12, 2025.
Watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kumuua Rhoda (42) kwa kumkatakata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na kusababisha kifo baada ya kumvamia nyumbani kwake kijijini hapo.
Wakili wa Serikali, Joyce Matimbwi ameeleza mahakamani hapo leo Jumanne Februari 3, 2026 kuwa, tukio hilo la mauaji lilitokea Oktoba 23, 2025 usiku.
Amesema washtakiwa hao walifika nyumbani kwa Rhoda kwa lengo la kufanya tukio hilo.
Amesema baada ya kufanikiwa kuingia ndani, watuhumiwa hao walimkatakata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na kusababisha kifo cha Rhoda aliyekuwa mkulima, kinyume cha sheria za kanuni ya adhabu kifungu cha 196 na 197.
Hata hivyo, Wakili Matimbwi amesema upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya shauri hilo kuja mahakamani hapo tena kwa ajili ya kutajwa.
Chanzo; Mwananchi