Zaidi ya madereva 100 wa malori kutoka Tanzania wamekwama Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) kufuatia tishio la kiusalama.
Madereva hao ambao kwa mujibu wa waliozungumza na Mwananchi wamezuiwa kuendelea na safari kutokana na vurugu za wananchi dhidi ya Serikali ya nchi hiyo.
Wamesema vurugu hizo zimeripotiwa leo Jumanne Januari 6, 2026 zikiwahusisha wachimbaji wadogo wa madini kufuatia tamko la Serikali kuwazuia kufanya shughuli zao.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, mmoja wa madereva hao, Frank Egina amesema madereva waliokwama katika Mgodi wa Kisamu wamejikuta katika hali hiyo kutokana na kutoweka kwa hali ya amani iliyosababisha shughuli zao kusimama na kuwalazimu kubaki bila uhakika wa usalama wao.
"Wachimbaji wadogo kwa kugomea tamko la Serikali wameamua kufanya fujo, mimi nilifika huku Jumapili na kufanikiwa kushusha mzigo vizuri, lakini leo nipo hapa Kisamu tumezuiwa kutoka mpaka hali itakaporejea," amesema Egina.
Hassan Maganga, dereva mwingine anayefanya safari zake kutoka Dar es Salaam kwenda DRC amesema hali ni mbaya katika mitaa ya eneo hilo huku usalama ukibaki sehemu ya mgodini walipokaa wakiwa katika ulinzi mkali wa vyombo vya ulinzi na usalama vya Taifa hilo.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Januari 6, 2026, kwa njia ya simu kuhusu changamoto zinazokabili madereva, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo amesema kuwa, hatua mbalimbali tayari zimeshachukuliwa ili kuhakikisha usalama na ustawi wa madereva hao, huku akisisitiza umuhimu wa kushirikiana na mamlaka husika ili kuondoa vikwazo vinavyokwamisha shughuli zao.
Chanzo; Mwananchi