Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Singida umetahadharisha wananchi kuacha tabia ya kuiba alama za barabarani, hasa riflekta na vyuma vilivyowekwa kwenye madaraja, kwa kuwa kitendo hicho kinasababisha hasara kubwa kwa serikali ambayo hutumia fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Singida, Mhandisi Dastan Singano, alitoa onyo jana wakati akitoa taarifa ya mradi kwa waandishi wa habari waliotembelea daraja la Konkilangi lililoko katika Kata ya Ntwinke, Wilaya ya Iramba, lililojengwa kwa gharama ya Sh. bilioni 7.
“Natoa wito kwa wananchi kutunza daraja hili kwani serikali imetoa fedha nyingi, takribani Sh.bilioni 7. Tunzeni miundombinu, msiibe alama za barabarani, vyuma vya kingo na riflekta,”amesema.
Singano alisema wapo baadhi ya watu wanaoiba riflekta zilizowekwa kwenye madaraja na kuziweka kwenye baiskeli zao jambo ambalo ni hatari sana kwani alama hizo zimewekwa kwa ajili ya usalama wa watu hususani nyakati za usiku.
Chanzo; Nipashe