Kufuatia tukio la Veronica Muhale (40), mkazi wa Wilaya ya Hanang’, mkoani Manyara, kudaiwa kumjeruhi vibaya mume wake, Josephati Kasi maarufu kama Khalidi Kasi (45), kwa kumkata sehemu za siri kutokana na wivu wa kimapenzi, mwandishi wa Global TV Hosea Elnino, amezungumza na wanafamilia wakiwemo watoto wa wanandoa hao.
Kwa mujibu wa simulizi za watoto, mara kadhaa mama yao amekuwa akijaribu kumdhuru baba yao. Walieleza kuwa kuna wakati mama aliwahi kumtuma mtoto wao wa mwisho dukani akanunue sumu ya panya akikusudia kumwekea baba yao, lakini jaribio hilo lilishindikana. Aidha, walidai pia kuwa siku nyingine mama yao aliwaagiza kumnunulia kisu na baadaye kukificha chini ya kitanda bila kueleza matumizi yake.
Watoto hao wamesema hawakuwahi kushuhudia wazazi wao wakigombana hadharani. Hata hivyo, wanaamini mama yao huenda hakutekeleza tukio hilo peke yake kutokana na changamoto za kiafya ambazo alikuwa akizipitia.
Kwa sasa, watoto wamesema wanaishi kwa hofu na changamoto kubwa za kimaisha, kwani baba yao ndiye alikuwa tegemeo la familia na kwa sasa amelazwa hospitalini kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata. Wameomba hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya mama yao, huku wakiiomba jamii na wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia.
Chanzo: Global Publishers