Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limeweka wazi kuwa litawafuatilia wanafunzi 19 walioandika matusi kwenye mitihani ya upimaji ya kitaifa ya darasa la nne na kidato cha pili iliyofanyika 2025 na kuhakikisha shule zinawachukulia hatua za kinidhamu.
Hatua hiyo inakuja kufuatia kukithiri kwa vitendo vya watahiniwa kuandika matusi kwenye mitihani, ambapo imeelezwa kuwa hawataishia kufutiwa matokeo yao bali watafuatiliwa na kuchukuliwa hatua zaidi.
Katika matokeo ya mtihani upimaji wa kitaifa wa darasa la nne uliofanyika Oktoba 2025, imebainika wanafunzi wanane wameandika matusi kwenye mitihani, wakati kwa upande wa kidato cha pili waliofanya kosa hilo ni 11.
Akizungumza leo Januari 10,2026 Katibu Mtendaji wa Necta, Profesa Said Mohamed amesema ufuatiliaji huo utafanyika kwa kuandika barua kwa wakuu wa shule husika za wanafunzi hao kwa kuwa bado wako kwenye mfumo wa shule.
“Tutaandika barua kwa mamlaka zao ikiwemo wakuu wa shule na bodi za shule au kamati za shule kwa ngazi ya shule za msingi, ikiwahusisha wazazi kuchukua hatua ili kuhakikisha suala la kuandika matusi linakomeshwa kabisa.
“Ukiangalia takwimu zetu, ni kweli sasa tunaanza kuona matusi kwa wanafunzi wa ngazi ya darasa la nne, mwaka jana tulikuwa na wanafunzi watano ila mwaka huu wamefika wanane, kwa sababu hawa bado wako kwenye mfumo wa elimu tutachukua hatua,” amesema Profesa Mohamed.
Chanzo; Mwananchi